Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA), ni asasi maalum ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM) ambayo ina mamlaka ya kuratibu shughuli za kukuza maendeleo na matumizi ya Kiswahili kikanda na kwingineko. Kiswahili kimepitishwa kuwa lugha rasmi ya JAM pamoja na Kiingereza na Kifaransa. Ili kuunga mkono matumizi yake kwa ufanisi katika mazingira ya wingi-lugha, KAKAMA inafanya utafiti ili kutathmini huduma za tafsiri na ukalimani wa Kiswahili katika Nchi Wanachama wa JAM. Lengo la utafiti huu ni kutathmini uwezo na utendakazi wa wataalam wa tafsiri na ukalimani wa Kiswahili ili kubaini changamoto na fursa za kuboresha huduma za tafsiri na ukalimani wa Kiswahili. Mchango na maoni yako yatachangia katika uendelezaji wa huduma za tafsiri na ukalimani katika JAM. Majibu yote yatahifadhiwa  kwa usiri wa hali ya juu na yatatumika kwa lengo la utafiti tu. Mchango wako unathaminiwa sana na utasaidia katika kuendeleza malengo ya kukuza Kiswahili kama lugha rasmi na lugha ya mawasiliano mapana katika JAM.