Maadhimisho ya 5 ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani na Kongamano la 3 la Kimataifa la Kiswahili Yatangazwa
0Years
0Months
0Days
0Hrs
0Mins
0Secs
Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) imetangaza rasmi kufanyika kwa Maadhimisho ya 5 ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani pamoja na Kongamano la 3 la Kimataifa la Kiswahili yatakayofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 7 Julai 2026 jijini Bujumbura, Burundi (JISAJILI HAPA)
Matukio hayo mawili yatafanyika chini ya kaulimbiu inayosema “Kiswahili, Wingi-lugha, na Akiliunde”, yakilenga kujadili nafasi ya Kiswahili katika ulimwengu wa teknolojia, akiliunde (AI), na jamii za wingi-lugha. Kwa mujibu wa waraka wa dhana (PAKUA HAPA), maadhimisho hayo yatatoa jukwaa kwa wanaisimu, wataalamu wa teknolojia, watunga sera, vijana na wadau mbalimbali kujadili namna Kiswahili kinavyoweza kuendelea kukua na kushindana kimataifa katika enzi ya kidijiti.
Kongamano hilo pia litaangazia matumizi ya akiliunde katika maendeleo ya Kiswahili, ikiwemo tafsiri za mashine, utambuzi wa lugha, mazungumzo ya kidijiti, pamoja na uundaji wa rasilimali za lugha za Kiafrika.
Mada ndogo zitakazojadiliwa ni pamoja na:
-
- Kiswahili na mustakabali wa kidijiti,
-
- Teknolojia ya lugha na elimu ya Kiswahili,
-
- Rasilimali za data za Kiswahili,
-
- Sera za lugha na teknolojia,
-
- pamoja na uhifadhi wa lugha za Kiafrika kupitia akiliunde.
Kwa ajili ya Kongamano la 3 la Kimataifa, Kamisheni ya Kiswahili inatoa wito wa ikisiri zisizozidi maneno 200 kwa Kiswahili au Kiingereza kuhusu mada ndogo yoyote kati ya zilizotajwa hapo juu au suala lolote linalohusiana na kaulimbiu ya Kongamano. Ikisiri zitumwe kwa kiskongamano@eachq.org ifikapo tarehe 30 Mei 2026. Waandishi wa ikisiri zitakazokubaliwa wataarifiwa ifikapo tarehe 10 Juni 2026. Ikisiri zilizofanikiwa zitaendelezwa kuwa makala ambazo zitachapishwa. Masuala na ufafanuzi wowote wa ziada kuhusu uandaaji wa kongamano yaelekezwe kwa jjowi@eachq.org